Upungufu wa madini muhimu
Ili nyanya iweze kustawi vizuri katika kila hatua yake ya ukuaji inahitaji virutubisho au madini muhimu, Panapokosekana madini hayo au virutubisho hivyo nyanya huweza kuonyesha dalili mbalimbali za upungufu wa madini husika. Yafuatayo ni madini au virutubisho na dalili zake endapo zitakosekana katika zao la nyanya.
1) Madini ya nitrogen (N)
Ni madini muhimu kwa ajili ya ukuaji hasa utengenezaji wa majani ya rangi ya kijani kibichi. Madini haya huitajika sana wiki chache baada ya kupandikiza. Rangi ya kijani ni muhimu kwa nyanya na hata kwa mazao mengine ili mmea uweze kutengeneza chakula chake.
Naitrogeni inapokosekana katika mmea rangi ya kijani hupauka na kuwa njano na hatimaye mmea kudumaa.
Pia naitrogeni inapotumika kwa wingi kupita kiasi husababisha mmea kuwa na majani mengi bila ya matunda na hivyo kuathiri matunda.
Kunapokuwa na upungufu wa naitrogeni inashauriwa kutumia mbolea za chumvi kama CAN, UREA, SA na NPK.
2)Madini ya fosforasi (P)
Ni madini muhimu katika utengenezaji wa mizizi na matunda kwa mimea na huitajika mara moja wakati wa kupanda, Inapatikana katika mbolea ya minjingu, DAP, TSP, NPK na n.k
Madini haya pia haipaswi kutumika kwa wingi kwani yakizidi huzuia mimea kuchipua kutoka ardhini.
Mmea wenye upungufu wa fosforasi majani yake na shina lake hubadilika rangi na kuwa rangi ya sambarau (purple) hasa sehemu za pembeni ya Jani . Ncha huinekana kama zimeungua na yale majani ya chini hubadilika na kuwa ya kahawia na mwisho kudondoka.
3) Madini ya potashi (K)
Ni muhimu wakati wa maua, matunda kwa mmea na kuimarisha ubora wa mbegu. Madini ya potashi pia huimarisha kinga ya mimea dhidi ya mashambulizi ya magonjwa mbalimbali.
Upungufu wa madini ya potashi huambatana na dalili kama vile majani huonekana kama yamebabuka kwa moto sehemu za pembeni ya Jani na majani kuwa ya njano katika mishipa yake ya pembeni. Dalili huanzia katika majani ya chini ya mimea na kupanda juu.
Dalili katika matunda ni kupauka yanapoiva na kutokua na rangi nyekundu iliyokolea.
Tumia mbolea aina ya minjingu, NPK au DAP katika kiwango husika ili kutatua tatizo hili
4) Madini ya magnesiam (Mg)
Ni madini muhimu katika kuhakikisha ubora wa matunda. Dalili za upungufu wa madini haya ni pamoja na majani kuwa na unene na uzito kupita kiasi, Pia mishipa katika majani kupoteza rangi yake asilia na kuwa na rangi ya kupauka. Upungufu hutokea hasa katika udongo wenye kichanga na tindikali nyingi (acid) na pia katika udongo wenye maji mengi kupita kiasi na katika hali ya ukame.
Mkulima anashauriwa kutumia mbolea ya magnesiam salfate ili kutatua tatizo hilo.
5)Madini ya kalisiam (CA)
Nyanya ni zao linalihitaji sana madini haya. Endapo madini haya yatapungua vitako vya matunda ya nyanya hubadilika rangi na kuwa nyeusi kisha husinyaa na kuoza, Aina mbalimbali za nyanya hutofautiana katika mahitaji ya madini haya.
Inashauriwa kutumia mbolea aina ya calcium nitrate (CAN) endapo madini haya yanapokosekana katika mmea.Pia mwagilia kwa wakati ili madini haya yaweze kusafirishwa vizuri.
ANGALIZO: Kabla ya kutumia Aina yoyote ya mbolea hakikisha unafata ushauri wa wataalamu.
Umwagiliaji katika nyanya
Nyanya ni zao linalihitaji maji mengi hasa wakati wa kupandikiza, Wakati wa kutoa maua na wakati wa kutoa matunda. Ni muhimu pia kua na uwiano mzuri wa umwagiliaji. Kunapokuwa na maji kidogo wakati wa matunda matatizo mbalimbali ya madini huweza kujitikeza kwa sababu madini hayo huyeyuka vizuri panapokua na maji ya kutosha.
Maji yanapokosekana katika nyanya hupelekea matunda kuoza na kupasukapasuka.
Matangazo (mulches)
Matangazo ya masalia ya mpunga, mahindi, mtama, migomba pamoja na nyasi kavu hutumika kufunika udongo shambani ili kupunguza upotevu wa unyevu pia matandazo husaidia kuzuia ukuaji wa magugu. Pia husaidia kuzuia upotevu wa joto la udongo.
Mzunguko wa mazao (crop rotation)
Kilimo cha mzunguko wa mazao ni muhimu kwani husaidia kupunguza maambukizi ya wadudu na magonjwa kwa mazao. Pia hutoa fursa kwa matumizi sahihi ya ardhi na udongo kwa sababu mazao hutofautiana katika matumizi ya madini ardhini.
Hivyo nyanya inashauriwa kufanyiwa mzunguko na mazao kama kabichi, vutunguu, maharage na karoti.
Hairuhusiwi kufanyia mzunguko na mazao ya jamii yake kama vile pilipili, burunganya, ngogwe, viazi mviringo na n.k
Wadudu wa nyanya
1)Nzi mweupe (whitefly)
Ni wadudu weupe wadogo wadogo wanaofanana na Nzi na huruka unapotikisa mmea. Wadudu hawa hushambuliwa kwa kufyonza maji maji ya majani, hasa majani machanga.
Pia wadudu hawa huweza kusambaza magonjwa ya virusi ambavyo ni hatari na hayana tiba
Udhibiti wa nzi weupe
Tumia viuatilifu vinavyoshauriwa na wataalamu, Usafi wa shamba na uondiaji wa masalia ya mazao na kuyachoma mara moja baada ya mavuno hupunguza kuzaliana kwa wadudu hawa na hivyo hupunguza mashambulizi.
Viuatilifu ambavyo husaidia kuua wadudu hawa ni kama Thiamex, Evisect 50 SP na Diazion pulizia majani na rudia kila baada ya siku saba.
2)Utitiri mwekundu (Red spider mites)
Hawa ni wadudu wadogo wenye rangi nyekundu hujilinda kwa utando kama buibui, Hawa hufanya uharibifu kwa kula majani hivyo majani huwa na madoa madoa madogo yenye rangi ya njano. Wadudu hawa pia hula matunda na kusababisha michubuko midogo yenye rangi ya njano au nyeupe iliyofifia.
Kudhibit Utitiri mwekundu
Tumia viuatilifu kwa kufuata maelekezo ya wataalamu, Usafi wa shamba na mazingira yake hasa kwa kuondoa magugu ya jamii ya nyanya kama vile ndulele na mnafu karibu na shamba.
Baadhi ya viuatilifu vinavyoweza kuua wadudu hawa ni kama Abalone 18 EC na Floramite 240 SC.
3) Wadudu mafuta/kimamba (Aphid)
Hawa ni wadudu wanaofyonza majimaji kwenye majani. Wana rangi mbalimbali kama vile nyeusi, kijani, njano na n.k na huwa na mbawa. Wadudu hawa pia husambaza magonjwa ya virus na pia husababisha unato unaopelekea ugonjwa wa masinzi (Soot mold) ambayo hutanda na kueka rangi nyeusi kwenye majani ya mimea, matunda na matawi.
Kudhibit
Tumia viuatilifu (Insecticides) kufuata maelekezo ya wataalamu. Miongoni mwa viuatilifu hivyo ni kama Cutter 112 EC, Attakan C 344 SE n.k
4) Funza wakataji (Cutworms)
Funza hawa ni wafupi na wanene hukaa ardhini. Wanaposhikwa na kuwekwa kiganjani hujikunja na kua mviringo. Wakati wa mchana hujificha ardhini na kuibuka wakati wa usiku na kukata mimea kichanga hasa wakati wa kupandikiza, Mashambulizi makubwa huonekana kwenye mashamba yenye magugu, yenye mboji nyingi hasa wakati wa mvua. Funza hawa hushambulia nyanya kabla kutoa matunda.
Kudhibiti
Viuatilifu vifuatavyo vinaweza kutumika kwa kufuata maelekezo ya wataalamu.
Cutter 112 EC, Crotale 46 EC na Diazion.
Dawa hizi zipuluziwe wakati wa jioni au usiku.
5)Funza wa vitumba (American bollworm)
Hawa hushambulia nyanya mara tu matunda yanapoanza. Hutoboa na kuingia katika matunda yanapokua madogo. Ni rahisi kuwadhibiti Funza hawa wanapokua wadogo lakini wanapokua wakubwa ni vigumu kuwazuia na mpaka mda huo wanakua wasababisha hasara kwa kutoboa matunda na kuyaozesha.
Kudhibiti
Miongoni wa viuatilifu vinavyoweza kuuwa Funza hawa ni Cutter 112 EC, Crotale 46 EC, Attakan C 344 SE n.k
Tumia kwa kufuata maelekezo ya wataalamu.
6) Minyoo fundo (Nematodes)
Ni Minyoo wadogo sana ambao huathiri mizizi kwa kuchimba ndani ya mizizi na kusababisha vifundo na mizizi kuvimba. Uvimbe na vifundo huathiri uwezo wa mizizi kunyonya maji na virutubisho kutoka ardhini, hivyo mimea kudhiofika, kunyauka, kudumaa na kushindwa kuzaa.
Kudhibiti
Panda Aina ya nyanya zinazostahimili (Resistant varieties) , tumia mzunguko kwa mazao kupunguza mashambulizi.
Pia dawa kama Furaban 3GR, Nemacur 5GR na Solvigo 108 SC zinaweza kutumika kwa kufuata maelekezo ya wataalamu.
7)Chorachora ( leaf minor)
Mabuu ya wadudu hawa hula majani ya nyanya na kutengeneza michirizi kama ramani. Michirizi hii pia huonekana kama machimbo ya mgodi. Michirizi hii hupunguza maji katika majani na hivyo kusababisha kudondoka pia hupunguza uwezo wa mmea kutengeneza chakula na kupunguza mavuno.
Kudhibiti
Viuatilifu kama vile Cutter 112 EC, FLORAMITE 240 SC huweza kutumika kwa kufuata maelekezo ya wataalamu.
8)Kanitangaze (Tuta absoluta)
Mdudu huyu kwa mara ya kwanza aliripotiwa Tanzania mwaka 2014 mdudu huyu huweza kula majani, shina na matunda, Kwahiyo huweza kusababisha hasara asilimia 100.
Huyu mdudu ni sugu kwa viuadudu vingi, Kuna viuadudu maalumu kwa huyu mdudu na hivyo vikitumika kwa mda mrefu mdudu huyu hujenga usugu. Mdudu huyu ana hatua nne za ukuaji na hatua ambayo ni hatari ni Ile ya Funza/ kiwavi kwani huaribu mimea.
Udhibiti
Viuatilifu kama CUTTER 112 EC, CROTALE 46 EC, EVISECT 50 SP ( hii huonenakana kuleta athari chanya zaidi ya viuadudu vingine) pulizia kila baada ya siku saba na jaribu kubadilii badili viuatilifu kwani ukitumia Aina moja kwa mda mrefu hujenga usugu wadudu hawa.
Comments
Post a Comment